Breaking News:

Top Ad

//

Naishukuru Simba Kwasababu Ilionesha Nia Ya Kunihitaji -Niyonzima





DAR ES SALAAM, Tanzania -Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba, Haruna Niyonzima amesema kuwa ana furaha kubwa kujiunga na klabu ya Simba huku akiwashukuru Wana msimbazi kwa mapokezi makubwa ambayo wamempa.
Niyonzima ametambulishwa rasmi kwa mara ya kwanza akiwa kama mchezaji wa Simba mbele ya mashabiki lukuki waliojitokeza uwanja wa taifa kwenye tamasha la Simba Day hapo jana ambapo walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Rayon Sport kutoka nchini Rwanda.
Akiongea na SportPesa News moja kwa moja baada ya kumalizika kwa mchezo huo ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Mohamed Ibrahim ‘Mo’ dakika ya 15, Niyonzima alisema kuwa amefarijika sana kwa mapokezi aliyoyapata kutoka kwa mashabiki.
“Namshukuru Mungu kwa mchezo wa leo, mimi ni mchezaji kwahiyo kujiunga na Simba ni furaha kwasababu ni timu ambayo imeonesha kunihitaji na najua nitakuja kufarijika nayo.
“Nawashukuru mashabiki wa Simba kwasababu haikuwa kitu rahisi lakini wameweza kunionesha ushirikiano na mapenzi, ni kitu ambacho na mimi pia kama mchezaji kinanipa morali”, alisema Niyonzima.
Sio Rahisi
Niyonzima alienda mbali na zaidi na kuzungumzia sakata lake la kuhama kutoka Yanga kwenda Simba ambao amesema haikuwa rahisi.
“Unajua siku zote kutoka Yanga kwenda Simba sio kitu rahisi lakini yote ni maisha na kwangu naweza kusema imekuwa kama ni hatma yangu kwahiyo niwaahidi kuwa mimi nimekuja kuwafanyia kazi na naamini kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu na kuwasikiliza walimu nitaweza kufanya vizuri.
Ubingwa
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Rwanda maarufu kama ‘Amavubi’ alikisifia kikosi cha Simba na kusema kuwa kimesheheni wachezaji bora na anaamini kuwa watatwaa ubingwa msimu ujao.
“Kikosi cha Simba ni kizuri na naamini mwaka huu tutafanya vizuri kwasababu tuna wachezaji wenye uzoefu ambao wanajitambua hivyo timu ni nzuri sana.
“Mimi sio Mungu siwezi kutabiri kama tutatwaa ubingwa lakini ukiangalia kikosi chetu haina budi kuchukua ubingwa wa ligi msimu ujao na naamini kwa uwezo wa Mungu tutafanya hivyo”, alimalizia Niyonzima.

Post a Comment

0 Comments